Saturday, August 1, 2015

Nape anaswa na Takukuru

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Lindi, imemhoji Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kwa madai ya kukutwa na fedha zinazodaiwa za kuwapa wajumbe ili wamchague katika kura za maoni.
Tukio hilo limetokea jana eneo la la Benki ya NMB saa 4:30 asubuhi.
Nape alikamatwa wakati akitoka ndani ya Benki hiyo, na alipofika nje alikutana na askari wa kikosi hicho, waliokuwa wamevalia kiraia  na kumuweka chini ya ulinzi.
Maofisa hao walimchukua kwa mahojiano ofisi ya Takukuru yaliyochukua saa tano, kuanzia saa 4:30 asubuhi hadi saa 9:30 alasiri na kuachiwa.
Waandishi wa habari waliokuwepo eneo hilo, walishuhudia askari hao wakimkamata na Nape kujaribu kupinga.
“Mheshimiwa sisi ni askari wa Takukuru, usijivunjie heshima tunakuomba uongozane na sisi kuelekea ofisini kwetu,” alisikika mmoja wa askari hao akisema.
Hata hivyo, hajaifahamika kiwango cha fedha zinazodaiwa kuchukuliwa na mgombea kutoka kwenye benki hiyo.
Waandishi wa habari walipomhoji Nape kuhusu tuhuma hizo, alikiri kwenda ofisi hizo, lakini alikataa kueleza alichoitiwa na kudai alikwenda kwa ajili ya matembezi yake binafsi.
“Mimi sikuhojiwa na Takukuru ila nilikwenda kwa matembezi yangu binafsi,” alisema Nape.
Kamanda wa Taasisi hiyo, Stephen Chami, alipotakiwa kuthibitisha tuhuma hizo, aliwataka waandishi wafanye subira, kwani wapo katika mahojiano nae.
Hata hivyo, baada ya saa nne kupita, mwandishi wa habari hizi alimpigia simu na kukiri kumhoji Nape.
Alisema katika mahojiano hayo, Nape alisema fedha hizo alizichukua  kwa ajili ya kuwalipa wakala.
Nape ametangaza nia ya kugombea jimbo la Mtama mkoani Lindi. Jimbo hilo lilikuwa linashikiliwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Bernard Membe. 
Chanzo: Nipashe

No comments :

Post a Comment