Thursday, August 13, 2015

NLD ;" UKAWA HAUNA MANUFAA"

UAMUZI wa umoja wa vyama vinne vya upinzani nchini (UKAWA) wa kuachiana majimbo, umezua balaa mkoani
Mtwara. Hali hiyo imetokana na uongozi wa Chama cha National League for Democracy (NLD), kudai uongozi wa Ukawa kuanzia wilayani hadi taifa umejawa na viongozi wabinafsi na wenye mizengwe.



Mwenyekiti wa NLD Mkoa wa Mtwara, Ahmed Nannyoho, alisema jana kuwa Ukawa ndani ya NLD hauna manufaa yoyote na wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi wa kishindo bila hata kuwa ndani ya Ukawa.



Amesema kuwa Mwenyekiti wao wa Taifa, Dk Emmanuel Makaidi, analitambua hilo licha ya kuendelea kushiriki katika mikutano ya Ukawa. Alitoa kauli hiyo wilayani Masasi jana, alipozungumza na vyombo vya habari baada ya kutakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu idadi ya wagombea waliojitokeza kugombea ndani ya NLD mkoani Mtwara.

Ukawa unaundwa na vyama vya NLD, NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema, na kwa mujibu wa makubaliano ya wakuu wa vyama hivyo, wataachiana majimbo katika mikoa mbalimbali nchini.

Mwenyekiti huyo wa NLD Mtwara alisema chama hicho kinatangaza rasmi kuwa hakiko tayari kuendelea na Ukawa, kwa madai kuwa umoja huo kuanzia Wilaya ya Masasi hadi ngazi ya Taifa, umejawa na viongozi wenye mizengwe na wenye ubinafsi, badala ya kujenga hoja za kuwatetea wananchi.

Alisema kuanzia sasa NLD inatangaza rasmi kwa wanachama wake wa Mtwara kuwa kinajitoa rasmi Ukawa, kwa sababu kimeona viongozi mkoani humo wamejawa na mizengwe katika kuendesha shughuli mbalimbali za Ukawa.

Alisema mfumo wa Ukawa ni kugawana majimbo na si kama uongo unaosambazwa na viongozi wa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi mkoani Mtwara kuwa wagombea wanaopaswa kugombea ubunge majimbo ya Ndanda, Masasi na Lulindi ni wa vyama hivyo na si wa NLD, kama ilivyokubaliwa kwenye vikao vya Ukawa Taifa.

Alisema viongozi wa Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF wilayani Masasi, wamekuwa wakijifanya wababe wa Ukawa na wamekuwa wakitoa taarifa za uzushi kwa wananchi, mazingira yaliyosababisha NLD kuvunja ukimya kwa wanahabari kuwa chama kilichopewa dhamana ya kusimamisha wagombea katika majimbo hayo ni NLD pekee.

Makaidi, mkewe wagombea ubunge Mwenyekiti huyo aliwataja wagombea wa NLD watakaosimama kugombea ubunge katika majimbo matatu ya Masasi kuwa ni Dk Makaidi (Masasi), Modesta Makaidi ambaye ni mke wa Dk Makaidi (Lulindi) na mgombea aliyemtaja kwa jina moja tu la Profesa Mpelumbe atakayejitosa jimbo jipya la Ndanda.

Alisema Ukawa ndani ya NLD, hauna manufaa yoyote, na wao wamejipanga kupata ushindi wa kishindo bila kuwamo humo, jambo alilodai Dk Makaidi analitambua licha ya kuendelea kushiriki katika mikutano ya Ukawa.

Alitoa mwito kwa wananchi mkoani Mtwara, kuacha kudanganywa na viongozi wa CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi na kushangazwa na kuona wamekuwa mstari wa mbele kujitokeza kujinadi kuwania majimbo hayo.

“Sisi NLD tunatambua wazi kuwa Ukawa tangu umeanza hasa kwa Wilaya ya Masasi, viongozi wake wamekuwa wakikihujumu chama chetu na kutangaza kuwa mgombea wetu, hana mvuto kwa wananchi kutokana na umri wake kuwa mkubwa licha ya kuwa elimu yake ni ya kutosha…sasa hujuma kama hizi hatuzikubali,” alisema Mwenyekiti huyo.

Aidha, Nannyoho alivigeukia vyombo vya habari, akisema hawako tayari kushirikiana na wanahabari katika kutangaza shughuli zake, kutokana na kuamini kuwa waandishi mkoani humo wamekuwa wakishirikiana na vyama vingine vinavyounda Ukawa, kueneza habari hizo za kutosimamisha wagombea.

Kauli ya Makaidi Akizungumza kwa njia ya simu kutoka jijiji Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama cha NLD Taifa, Dk Makaidi, alikiri ni kweli kuwa vyama vya siasa vinavyounda Ukawa kupitia vikao vyake halali, wamekubaliana NLD kisimamishe wagombea kwenye majimbo matatu ya uchaguzi ya wilayani Masasi, ambayo ni Ndanda, Lulindi na Masasi.

Alisema kimsingi maamuzi hayo yako wazi, licha ya kushangazwa kwake na baadhi ya wanachama wa vyama vya CUF na Chadema, kuendelea na kampeni za kuomba ridhaa kwa wananchi, wachaguliwe kwenye nafasi hizo za ubunge.

Chama kingine kwenye umoja huo ni NCCR-Mageuzi. “Ndugu mwandishi nashangazwa na kinachoendelea huko Masasi, kwani huku juu tayari tumemaliza na makubaliano tumefikia…lakini cha ajabu nasikia jana kuna mgombea wa CUF, Ismail Makombe (Kundambanda) amechukua fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Masasi kwa madai eti anapendwa sana na wananchi wa jimbo hilo,” alisema Dk Makaidi.

Akizungumza kuhusu kashfa na kejeli alizozitoa Mwenyekiti wake wa mkoa wa Mtwara, alisema alichofanya mwenyekiti huyo, si kitendo cha kiungwana kwa waandishi wa habari huku akiomba radhi na kuahidi kumpigia simu kumuonya.

Alisema kwa kitendo alichokifanya mwenyekiti huyo, kimempa shaka ya hata namna ya uongozi wake kwenye chama hicho mkoani humo. Alisema kwamba atakaa na kamati ya nidhamu ya chama, kuona namna watakavyomuadhibu mwenyekiti huyo. Kuhusu kujitoa kwenye Ukawa, Dk Makaidi alikana kuwa si kweli.

Alisema ana wasiwasi na utendaji kazi wa mwenyekiti huyo NLD mkoa wa Mtwara na kwamba atatoa taarifa rasmi namna alivyoshughulikia suala hilo.
CHANZO; Habari leo


No comments :

Post a Comment