Saturday, August 8, 2015

SERIKALI: "ulevi na uzembe mambo yanayochangia matukio ya uporaji silaha na mauaji ya polisi"

Serikali imesema matukio ya uporaji wa silaha na matukio ya mauaji ya askari wa Jeshi la Polisi nchini ya hivi karibuni, yanachangiwa na ulevi, uzembe katika doria pamoja na
kukaribisha watu wasiowajua.


Naibu waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima, alitoa kauli hiyo jana katika Shule Kuu ya Polisi-Moshi (MPA), wakati akifunga mafunzo ya awali ya askari 3,497 wa Polisi na Uhamiaji.

“Askari wetu wakati mwingine wanaonekana hawako makini katika utendaji wao wa kazi, lakini matukio ya uporaji wa silaha na mauaji ya askari yaliyotokea katika vituo vya Ushirombo, Stakishari, Mkuranga Mbagala na kwingineko ambako sijakutaja; ulevi na uzembe katika doria ni miongoni mwa mambo yanayoonekana kuchangia,” alisema Pereira. 

Awali, Mkuu wa Shule hiyo, Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP), Matanga Mbushi, alisema katika mafunzo hayo, askari tarajali 126, walifukuzwa kutokana na sababu mbalimbali.

“Kati ya hao, 193 walioachishwa mafunzo wanatoka polisi na askari tarajali 13 ni wa idara ya uhamiaji, lakini pia askari wawili walifariki dunia kutokana na maradhi. Hivyo kufanya idadi ya waliohitimu na kuajiriwa ni askari 3,497,”alisisitiza Matanga

Naibu mkuu wa jeshi hilo nchini, Abdulrahman Kaniki aliwaagiza wakuu wa vikosi vyote mikoani pamoja na makamanda wa polisi wa mikoa kuhakikisha askari waliomaliza mafunzo ya awali wanaendelea kupata elimu ya vitendo kwa muda wa miezi tisa kuanzia sasa.

Akizungumzia uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, Kaniki amewapiga marufuku askari wa Jeshi hilo kujihusisha na ushabiki wa kisiasa, kwa kujiingiza katika makundi ya wagombea nafasi za urais, ubunge na udiwani, huku akiwataka kuacha kufumbia macho uhalifu unaotendwa kwa kisingizio cha siasa.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment