Monday, August 3, 2015

Wagombea ubunge CCM Moshi Mjini wagoma kusaini matokeo.

Wagombea wawili wa kiti cha ubunge katika Jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ‘wamegoma’ kusaini matokeo ya kura za maoni yaliyompa ushindi
mfanyabiashara maarufu wa jijini Dar es Salaam, Davis Mosha.
Waliogoma kusaini matokeo hayo ni Buni Ramole na Patrick Boisafi, ambao walikuwa washindani wakuu wa Mosha kati ya wagombea 12 waliojitokeza kuomba kuteuliwa na CCM kugombea ubunge Jimbo la Moshi Mjini.
Katibu wa CCM Moshi Mjini, Loth Ole Nessele, aliliambia NIPASHE jana kwa njia ya simu kwamba Buni alikataa kusaini matokeo hayo akidai amepata `presha' kutokana na mchakato huo wakati Boisafi alimweleza kwamba hawezi kusaini kwa sababu yupo nyumbani peke yake na amechoka kutokana na mchakato huo.
Wagombea wengine kati yao ni Priscus Tarimo, Edmund Rutaraka, Shaniel Ngindu, Innocent Siriwa, Amani Ngowi, Omari Mwariko, Michael Mwita, Daudi Mrindoko na Khalifa Kiwango. 
Alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo, Buni alisem: “Ni kweli nimekataa kusaini matokeo na tayari nimewaandikia na kuwakabidhi CCM barua nikiwaeleza kuhusu uamuzi wangu. Rushwa za wazi wazi na upendeleo kwa mgombea mmoja ni hatari na wala CCM isifikiri kwa mwendo huu italikomboa Jimbo la Moshi Mjini,” alisema Buni.
Katika  uchaguzi wa kura ya maoni CCM, Buni aliongoza mwaka 2010 kwa kupata kura 1,554 dhidi ya Thomas Ngawaiya (1,539), Justine Salakana (1,152), Gibson Lyamuya (266), Onesmo Ngowi (127), Peter Chambi (110), Joseph Mwariko (109) na Joseph Mtui (208).
Hata hivyo, Salakana ndiye aliyepitishwa kuchuana na Mbunge wa sasa, Philemon Ndesamburo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Aidha, NIPASHE ilipomtafuta Boisafi kutoa ufafanuzi kuhusu hatua yake ya kudaiwa kususia kusaini matokeo ya uchaguzi wa kura ya maoni, hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuzimwa muda wote.
Wakati huo huo, watia nia sita wa ubunge Jimbo la Vunjo waliokuwa wakiomba kuteuliwa kuwania kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, wameuandikia barua uongozi wa CCM wakitaka kitoe adhabu kwa mtia nia aliyeshinda uchaguzi huo, Innocent Meleck.
Watia nia hao, Masiga Amos, Veronica Shao, Evelyine Msangi, Mchungaji Alphonce Temba, Joachim Kessy na Peter Msakcy, ambao walisaini barua hiyo Julai 25, mwaka huu na NIPASHE kuona nakala yake.
Nakala za barua hizo pia zimepelekwa kwa Katibu wa CCM Mkoa, Emmanuel Rutta na Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana.
Pamoja na mambo mengine, wanakitaka chama hicho kutoa adhabu stahiki baada ya kura za maoni la sivyo watatoa tamko lao kueleza uamuzi mgumu watakaouchukua.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment