Friday, August 7, 2015

WAZIRI MWINGINE AANGUKIA PUA

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani (pichani), amekuwa waziri wa tisa kuangushwa katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ameangushwa na Dk. Raphael Chegeni katika jimbo la Busega, baada ya kupata kura 11,829 dhidi ya 13,048 za Dk. Chegeni.

Awali matokeo hayo yalikuwa na mizengwe kwa madai ya kuwapo na uchakachuaji na kuilazimisha CCM kuingilia kati kupitia upya kura hizo.

Katibu Jumuiya ya Wazazi wilayani humo, William Bandeke, kwa niaba ya katibu wa wilaya hiyo, andiye aliyetangaza matokeo hayo jana bna kumaliza mvutano uliokuwa umeibuka.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa, Dk. Chegeni alisema ushindi huo umeonyesha jinsi gani wananchi wa Busega walitaka kudhulumiwa haki yao.

Dk. Chegeni alionya ngazi ya mkoa isitumie mizengwe ya kumbeba mtu ambaye hakushinda, iache vikao vya maamuzi vifanye kazi yake na kuomba wapinzani wake wamuunge mkono.

“Unaweza kuiba kura kumbe unaharibu, nitoe wito kuwa watu wakubali matokeo na hii ndiyo demokrasia na iwe mwiko mtu kupora haki ya mtu, kazi hapa imekwisha, naasubiri vikao vya juu vifanye maamuzi,” alisema Dk. Chegeni.

Alisema sababu kubwa ya kushindi wake imetokana na kazi aliyoifanya akiwa mbunge.

“Siasa ni kazi ngumu, niombe wagombea wenzangu waniunge mkono, maana sasa mimi ndiye naweza kupeperusha bendera ya chama. Lakini Niwashukuru wananchi na wana CCM wa Busega, wamenitendea haki nami nawaahidi sitawaangusha,” alisema Dk. Chegeni.

Dk. Kamani mbali na ubunge alikuwa akiwania nafasi ya urais kupitia CCM, lakini hata hivyo kura hazikutosha mchakato ambao Dk. John Magufuli aliiibuka mshindi.


Mawaziri walioanguka katika kura za maoni ni waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Maathias Chikawe; Naibu waziri wa Fedha, Adam Malima; Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga; Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka; Naibu waziri wa Maji, Amos Makala; naibu waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Maalima; Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pareira Silima na Naibu Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana.

No comments :

Post a Comment