Saturday, June 27, 2015

Mwandosya amuita Lowassa kambi yake

Dodoma. Profesa Mark Mwandosya, ambaye anawania kuteuliwa na CCM kugombea urais, amemtaka Edward Lowassa kujiunga na kambi yake kwa kuwa makada wengine wanne kwenye mbio hizo wanamuunga mkono.
Hata hivyo, wawili kati ya makada hao wanne wamekana kumuunga mkono.
Mwandosya, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), alisema tayari Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Steven Wasira, Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta na waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe wanamuunga mkono na hivyo kumshauri Lowassa kujiunga na kambi yake.
“Kama (wagombea) wengi wananiunga mkono, aliyebakia basi atakuwa ni ndugu yangu, rafiki yangu, Edward Lowassa. Naye angesema hivyo ingerahisisha sana kazi ya chama, ingepunguza sana kazi, makundi yangekuwa yameisha,” alisema Mwandosya baada ya kurejesha fomu za kuomba CCM impitishe kugombea urais.
“Halmashauri Kuu isingepata shida, Kamati Kuu isingepata shida nadhani tungeweza kufika pale ambako tungefika tarehe 12 (Julai, siku ambayo Mkutano Mkuu wa CCM utamchagua mgombea urais), bila kikwazo, bila makundi,”alisema mbunge huyo wa Rungwe Mashariki jana.
Lakini kauli yake imepokewa kwa hisia tofauti na watu hao aliodai wanamuunga mkono, huku kambi ya Lowassa ikizungumzia kauli hiyo kuwa si ya mtu aliye makini kwenye mbio za urais.
Jumla ya makada 40 wamechukua fomu za kuomba ridhaa ya CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25 na chama hicho kina kazi ngumu ya kumpata mwanachama atakayemrithi Rais wa sasa, Jakaya Kikwete ambaye katiba inamzuia kuendelee kuongoza baada ya kumaliza vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja.
Mgombea urais wa CCM pia ndio atakuwa mwenyekiti wa chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kurudisha fomu jana, Profesa Mwandosya alisema mchakato huo umewafanya wanaoomba urais kuwa marafiki zaidi licha ya kupigana vijembe, akisema ingekuwa nchi nyingine wangefanyiana vurugu.
Aliwashukuru wagombea wenzake waliotamka hadharani kuwa watamuunga mkono endapo hawatapitishwa na Kamati Kuu ya CCM kugombea urais.
“Namshukuru Benard Membe ambaye  ametangaza na kuandikwa (kwenye vyombo vya habari) kwamba yeye ameona katika orodha yote ya watu 40, kama si yeye basi ataniunga mkono mimi na yupo tayari kuzunguka nchi nzima iwapo chama kitaniteua kuwa mgombea,” alisema Profesa Mwandosya.
“Namshukuru pia Mheshimiwa Pinda, amelizungumzia hili katika vituo kama si kimoja viwili kuwa moyo wake utakuwa na furaha kama Profesa Mwandosya anaweza kuteuliwa na chama.”
Source: Mwananchi

No comments :

Post a Comment