Friday, June 26, 2015

Serikali yafuta vyuo vitatu

Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Elimu la Ufundi (Nacte) limefuta usajili wa vyuo vitatu na kuvishusha hadhi vingine 16 kutokana na kukiuka masharti ya usajili.

Vyuo vilivyofutiwa usajili ni Dar es Salaam College of Clinical Medicine, Ndatele School of Medical Laboratory Sciences, vinavyohusika na elimu ya tiba, na Institute for Information Technology kinachofundisha elimu ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Teknohama).

Akitangaza uamuzi huo jijini hapa jana, kaimu katibu mtendaji wa Nacte, Dk Adolf Rutayuga alisema vyuo hivyo vimeshindwa kurekebisha kasoro ambazo baraza hilo lilizibaini na kuvitaka kufanya marekebisho. Alisema baraza hilo lilitoa notisi ya siku 30 likivitaka vyuo vyenye upungufu katika usajili na ithibati kutoa maelezo na kufanya marekebisho.

Kaimu mkurugenzi huyo alisema baadhi ya vyuo vilifanya marekebisho kama vilivyoogizwa.

Alitaja makosa yaliyokiukwa kuwa ni kumalizika kwa muda wa usajili, kutoanza mchakato wa kupata uthibitisho wa kufikia viwango vilivyowekwa, kumalizika muda wa ithibati na kutoomba upya usajili pamoja na vyuo kuamua kusitisha mafunzo.

Alisema mbali na vyuo hivyo vitatu vilivyofutiwa usajili, vingine 16 vimezuiwa kusajili wanafunzi au kushushwa hadhi.

Alisema Darmiki College of Educational Studies imezuiwa kusajili wanafunzi baada ya kubainiki kinadahili bila kusajiliwa.

Alivitaja vyuo vilivyoshushwa hadhi kuwa ni Sura Technologies, Institute of Management and Information Technology, Techno Brain, Ministry of Agriculture Training Institute Igurusi, Mbozi School of Nursing, KCMC AMO Ophthalmology School, KCMC AMO Anaesthesia School, Advanced Pediatrics Nursing KCMC.

Vingine ni AMO Training Centre cha Tanga, CATC Sumbawanga, CATC Songea, COTC Maswa, COTC Musoma, Dental Therapists Training Center, Ngudu School of Environmental Health Sciences Kwimba na KCMC AMO General School Moshi.

No comments :

Post a Comment