Katibu wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Juma Shesha akimkabidhi Fomu, Jumaa Mhina ya kuomba kuteliwa na Chama hicho kuwania Ubunge jimbo la Kawe katika uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika oktoba. |
Dar/mikoani. Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) ameanza kuonja joto la kuwania ubunge katika jimbo hilo baada ya watu wanane kujitokeza kwa siku ya kwanza kuitaka nafasi hiyo.
Pia yumo Elias Nawela, Dk Walter Nnko, Atulinda Barongo, Tegemeo Sambili, Shuganga George na Edmund Lyatuu.
Mdee amekuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia Chadema tangu mwaka 2010, lakini sasa atakuwa na kazi ya kupambana na baadhi ya makada hao wa CCM waliochukua fomu kulitaka jimbo hilo.
Wengine katika maeneo mbalimbali nchini waliochukua fomu ni pamoja na Moshi Mjini ambako makada wa CCM wameanza kupigana vikumbo kutaka kumrithi mbunge wake wa sasa, Philemon Ndesamburo.
Kada wa kwanza aliyechukua fomu ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Mwita na wafanyabiashara, Davis Mosha na Patrick Boisafi.
Mjini Mbeya, Mwenyekiti wa UVCCM, Amani Kajuna ameibuka na kutaka kuwania ubunge Jimbo la Mbeya Mjini.
Katika Jimbo la Kinondoni Idd Azzan anayetetea jimbo lake anatarajiwa kuchuana na Wangota Salum, John Kalinjana na Goochange Msangi wakati Ubungo Didas Masaburi na Joseph Massana wamejitokeza kumvaa John Mnyika.
Katika Jimbo la Kibamba waliojitokeza ni George Shija, Dk Meshack Sabaya, Dk Fenella Mukangara na Rashid Kikazi.
Wanaowania kupitia viti maalumu Kawe ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angela Kairuki, Zarina Madabida, Getrude Lwakatare, Florence Masonga, Mary Daffa, Warda Maulid, Anna Matulu, Emelda Mwananga, Maria Kigalu, Angela Kizigha na Ummy Nderiananga.
Mkoani Dodoma, mbunge anayemaliza muda wake, David Malole na anayemiliki Kiwanda cha Magodoro ya Dodoma asili, Haidari Gulamali wamejitokeza kuchukua fomu pia.
Jimbo la Chilonwa waliojitokeza ni pamoja na Joel Makanyaga, Daniel Ligoha, Anderson Magolola, Deo Ndejembi na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Pololeti Mgema na Dk Kedimon Mapana.
Mbunge aliyemaliza muda wake, Hezekia Chibulunje ameshatangaza kutowania. Jimbo la Mtera Livingstone Lusinde ametangaza kuendelea huku akikutana na upinzani kutoka kwa mtoto wa waziri mkuu mstaafu, John Malecela, Samweli Malecela, Lameck Lubote, Stephen Ulaya na Philip Elieza.
Ukonga nako Jerry Silaa hatimaye amechukua fomu sambamba na Jackob Katama, Hamza Mshindo, Frederick Rwegasira, Anthony Kalokola, Ramesh Patel na Peter Majura wakati Jimbo la Ilala aliyechukua fomu ni Mussa Hassan Zungu pekee mpaka jana.
Jimbo la Segerea linawaniwa na Zahoro Lyasuka, Apruna Humba na Bona Kalua huku Kigamboni Harun Rashid Othman ndiye aliyechukua fomu na Mbagala waliojitokeza ni Lucas Mashauri Malegeli, Mindi Mohammed Kuchilungulo, Kazimbaya Makwega, Adadius Richard, Tambwe Hiza, Issa Ally Mangungu, Ingawaje Kajumba na Siagi Ngega Kiboko.
Jimbo la Temeke Abbasi Zuberi Mtemvu anaendelea kutetea nafasi yake, akijiandaa na upinzani kutoka kwa Joseph Wilbert Mhoha, Khamis Salim na Maimuna Hassan Kayanda.
Njombe Kusini, waliochukua ni Edward Mwalongo, Alfred Luvanda na Arnold Mtewele wakati Njombe Kaskazini; Laula Malekela, Emmanuel Kilundo na Joramu Hongoli ndiyo waliochukua fomu.
Makambako aliyejitokeza ni Alimwinike Sahwai.
Waliojitokeza kumrithi Profesa Mark Mwandosya Rungwe Mashariki ni Ezekiel Gwatengile na Rungwe Magharibi ni Mhandisi Charles Mwambene.
Katika Jimbo la Arusha Edmund Ngemela ndiye aliyechukua fomu.
Kibaha Mjini ni Rugemalira Rutatina anayelitaka jimbo linaloshikiliwa na Silvester Koka.
Wakati huohuo, Jiji la Mwamza jana lilizizima wakati Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje alipokwenda kuchukua fomu za kuwania nafasi hiyo kwa tiketi ya Chadema.
Shughuli zilisimama kwa muda wakati wa kwenda kwenye ofisi za wilaya za chama hicho na kurudi katika Uwanja wa Mbugani kuhutubia mkutano wa hadhara huku barabara zikifungwa kutokana na msafara wa magari na pikipiki zilizokuwa zimemsindikiza .
No comments :
Post a Comment