Wednesday, July 29, 2015

Hotuba kamili ya Lowassa kujiunga Chadema

Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa akionyesha
Ndugu waandishi wa habari na ndugu Watanzania wenzangu.
Yamepita majuma mawili tangu mchakato wa kuchagua mgombea urais wa Tanzania
kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) ukamilike. Nimetumia muda huu kutafakari kwa kina yaliyotokea Dodoma na hatima yangu katika siasa nchini. Ninajua marafiki wengi na wananchi wenzangu wanaoniunga mkono wamekuwa wakisubiri kwa hamu nitoe kauli.
Nilipokuwa natangaza nia ya kugombea urais kule Arusha, nilieleza nia yangu ya kuanza mchakamchaka wa maendeleo ya nchi yetu na kuondokana na umaskini. Pamoja na yaliyotokea Dodoma, azma hii bado iko palepale.
Lakini nianze kwa kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetupa sisi pumzi ya kuendelea kuwa wazima wa afya njema hadi hivi sasa. Nawashukuru pia mke wangu Regina, wanangu, wanafamilia na marafiki wote kwa mapenzi, msaada na uvumilivu wao wakati wa kipindi hiki kigumu tunachopitia. Nawashukuru sana pia maelfu ya wanachama wa CCM walionidhamini na mamilioni zaidi walioniunga mkono.
Katika safari zangu za mikoani wakati wa kuomba udhamini, nilitiwa hamasa na umati mkubwa wa watu waliojitokeza kuniunga mkono.Aidha, ninawashukuru sana wana kamati wangu, makundi mbalimbali na mamilioni ya vijana wakiwamo; “For You Movement”, “Friends of Lowassa” “Team Lowassa”, Umoja wa Bodaboda na wengine wengi ambao walijitolea kwa hali na mali katika Safari yetu ya Matumaini.
Nitakuwa sijahitimisha orodha ya shukrani iwapo nitaacha kuwashukuru viongozi wa dini zote nchini ambao waliungana na waumini wao wengi katika maombi na kwa kuniunga mkono. Najua sote tumevunjika moyo kwa yaliyotokea Dodoma na mazingira yaliyopelekea matokeo yale.
Kama ilivyokwishaelezwa, mchakato wa kuteua wagombea uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjaji wa Katiba na taratibu za uchaguzi za CCM.
Zaidi ya hayo uchaguzi ulisimamiwa kwa upendeleo dhahiri na chuki iliyokithiri dhidi yangu. Kikatiba, Kamati ya Maadili si chombo rasmi na haina madaraka ya kuchuja na kupendekeza majina miongoni mwa wale wanaoomba kugombea Urais kupitia CCM.
Kilichotokea Dodoma ni kupora madaraka ya Kamati Kuu na kukiuka katiba ya CCM. Aidha, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu viliitishwa na kuburuzwa ili vitekeleze azma ya watu binafsi pasipo kujali demokrasia, katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM. Niliwekewa mizengwe na kuzushiwa majungu na uongo mwingi, kuhakikisha kuwa jina langu halifikishwi mbele ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kujadiliwa licha ya ukweli usiopingika kuwa nilikuwa mgombea anayeungwa mkono na wananchi na wanachama wengi wa CCM kuliko wenzangu wote. Kibaya zaidi ni kile kitendo cha kuwanyima wagombea wote 38 haki ya kujieleza mbele ya Kamati Kuu.
Ni dhahiri kwamba njama dhidi yangu ndani ya CCM si jambo jipya.Kumekuwa na mkakati wa siku nyingi wa kulichafua jina langu kwa uzushi na uongo usio na kifani. Aidha, mmeshuhudia jinsi vijana kadhaa walivyotumika kunikashifu na kunitukana na bila aibu na uongozi wa CCM na Serikali kuwazawadia madaraka makubwa.
Kwa namna ya kipekee napenda kuwapongeza na kuwashukuru wazee wetu akiwamo Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na baadhi ya  wajumbe wa Kamati Kuu ikiwa ni pamoja na waheshimiwa Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Alhaj Adam Kimbisa kwa uadilifu na ushujaa wao mkubwa wa kuisimamia katiba ya CCM na misingi ya haki na kukataa maamuzi batili ya Kamati ya Maadili na Kamati Kuu kuhusu uteuzi wa wagombea.
Cha msingi kuzingatia ni kuwa ili kuhitimisha njama za kunipora mimi na wagombea wengine haki zetu za msingi za kusikilizwa, viongozi wachache walikuwa tayari kupanda mbegu ya chuki na mfarakano ambao ni mfano mbaya kwa CCM na hata Taifa letu. Watanzania walitarajia chama kinachoongoza nchi kiwe ni mfano wa utawala wa sheria na kinara katika kutetea misingi ya haki na demokrasia na siyo kuihujumu. Yaliyotokea Dodoma yameitia dosari nchi yetu.
Kwa kifupi, ninaamini sikutendewa haki katika mchakato mzima wa kupendekeza majina na kuteua mgombea wa urais kupitia CCM. Nilinyimwa haki yangu ya msingi ya kusikilizwa na kuchaguliwa.
Kwa mantiki hii nitakuwa mnafiki kama nitaendelea kujidanganya mimi mwenyewe na umma wa Watanzania kwa kusema kuwa bado nina imani na CCM au kuwa CCM ni chama kitakachowaletea ukombozi wa kweli wa kiuchumi, kisiasa na kijamii. CCM niliyoiona Dodoma siyo tena kile chama nilichokulia na kilichonipa malezi na maadili ya siasa yaliyojengwa kwenye misingi ya haki, usawa na uadilifu.
Ni dhahiri kwamba CCM imepotoka na kupoteza mwelekeo na sifa ya kuendelea kuiongoza Tanzania yetu. Mimi kama Mtanzania aliye na uchungu na nchi yake nasema imetosha na SASA BASI!
Kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyosema, CCM siyo baba yangu wala mama yangu na kwamba kama Watanzania hawapati mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM. Sasa tuyatafute mabadiliko nje ya CCM.
Hivyo basi, baada ya kutafakari kwa kina nimeamua kuwa kuanzia leo ninaondoka CCM na kuitikia wito wa Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuungana nao katika kuleta mabadiliko ya kweli ya nchi yetu. Navishukuru vyama vyote vya siasa chini ya Ukawa, yaani Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kwa mwaliko wao na imani yao na kuthamini mchango ninaoweza kutoa kufanikisha azma ya kuleta mabadiliko na maendeleo ya kweli ya Taifa letu. Waheshimiwa Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, Mheshimiwa James Mbatia na Emmanuel Makaidi asanteni sana.
Ndugu zangu, sikuufanya uamuzi huu kwa pupa, lakini unafika wakati wa kuchukua maamuzi hata kama ni magumu  kwa kuamini fika kuwa ni kwa masilahi ya Taifa letu.
Nimejiridhisha kuwa ndani ya Ukawa Taifa letu linayo fursa ya pekee na ya kihistoria kushinda Uchaguzi Mkuu ujao na ya kuleta mabadiliko ya msingi katika nchi yetu. Kwa uamuzi na ushiriki wangu huu, ninaamini kwa dhati kuwa tutaondoa uhodhi wa madaraka wa chama kimoja na kujenga demokrasia yenye ushindani wa kweli kisiasa.
Namalizia kwa kutoa wito kwa Watanzania wenye nia njema na nchi yetu na wanaotaka kujenga demokrasia na kuleta mageuzi na maendeleo ya kweli, kujiunga nasi katika safari hii mpya ya kuinusuru nchi yetu.
Safari ya Matumaini inaendelea kupitia Ukawa lakini haitafanikiwa iwapo sote hatutajiandisha kupiga kura. Natoa wito kwa wakazi wa Dar es salaam, kutumia fursa iliyopo kujiandikisha kwa wingi.
Aidha, nawakumbusha Watanzania kote nchini waliojiandikisha kutunza shahada zao na kukumbushana kupiga kura ili ifikapo Oktoba mwaka huu tupate ushindi wa kishindo.
Ndugu zangu Watanzania, tuungane pamoja kuuondoa umaskini na kuleta mabadiliko ya kweli.
NARUDIA CCM SIYO MAMA YANGU

No comments :

Post a Comment