Monday, July 27, 2015

JAMES MBATIA APITA KURA ZA MAONI VUNJO BILA KUPINGWA

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia amepita bila kupingwa katika mchakato wa kumtafuta mgombea ubunge jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro kupitia chama hicho.
Mbatia amepitishwa baada ya vikao vya Kamati ndogo kwenye ngazi ya matawi, kata na jimbo kumpa alama ‘A’ sawa asilimia 100 baada ya kuwa mgombea pekee aliyejitokeza kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania ubunge.

Katibu wa NCCR Mageuzi jimbo la Vunjo, Mathew Temu alisema Mbatia alipitishwa na vikao hivyo wiki iliyopita hasa kutokana na mchango wake katika chama, uwezo na nia ya kulikomboa jimbo kutoka mikononi mwa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP).
Alisema Mbatia alichukua fomu na kuirejesha Juni 29, mwaka huu.

“Waliompitisha ni wajumbe wa kikao halali cha jimbo la Vunjo; kwa kuwa mchakato huo ulianzia kwenye ngazi za matawi na Kata,”alisema Temu.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya NCCR-Mageuzi, Hemed Msabaha alisema kamati ndogo zilipewa mamlaka ya kufanya uteuzi kwa niaba ya Halmashauri Kuu na hivyo jina la Mbatia lilishapitishwa rasmi.

Mbatia anakuwa kiongozi wa pili mwandamizi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupita bila kupigwa katika mchakato wa kura ya maoni ya kiti cha ubunge baada ya juzi wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi Wilaya ya Hai, kumchagua Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kwa kura 269.

Mbowe naye alipita bila kupingwa katika mchakato wa kura ya maoni ya ubunge wa jimbo la Hai, baada ya kuvuna kura 269 sawa na asilimia 98.2.

Wakati huo huo, Mkutano Mkuu Maalum Wilaya ya Mwanga, ulimchagua Hendry Kilewo kwa kura 109, kuwa mgombea wake wa kiti cha ubunge.

 Kada huyo aliwashinda Mdimu Ngoma aliyepata kura 25, Joyce Mfinanga kura 38, Mengi Kigombe kura 2 na Nurdin Jela aliyeambulia kura moja. 

No comments :

Post a Comment