Baada ya tetesi za muda mrefu, hatimaye Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi ), Moses Machali amejiunga na Chama cha ACT - Wazalendo.
Naibu Katibu Mkuu wa ACT - Wazalendo, Msafiri Mtemelwa alisema hayo jana alipokuwa akimtambulisha kwa waandishi wa habari, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitengo cha Vijana wa NCCR - Mageuzi, Deo Meck ambaye naye amejiunga na chama hicho.
Machali ambaye hakuwapo kwenye utambulisho huo, alithibitisha kwa simu jana kujiunga na chama hicho kipya kinachoongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na kusema atatoa ya moyoni Julai 21 katika mkutano utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kiganamo, Kasulu Mjini.
“Nitakuwa na Zitto na wabunge wengine ambao siwataji kwa sasa,”alisema Machali.
Awali, Mtemelwa alisema Machali amejiunga na chama hicho na kwamba kinachosubiriwa ni utaratibu maalumu wa kumtambulisha kwa wananchi.
Awali, Mtemelwa alisema Machali amejiunga na chama hicho na kwamba kinachosubiriwa ni utaratibu maalumu wa kumtambulisha kwa wananchi.
“Siyo Machali pekee ambaye amekuwa akihusishwa kuhamia katika chama hiki, bado kuna wabunge kama wanne, nao wakati wowote watatambulishwa kwa wananchi. Staili yetu kwa hawa wabunge ni kuwapokea na kuwatambulisha katika majimbo yao, mbele ya wapigakura,” alisema Mtemelwa.
Alisema kuhamia katika chama hicho kwa wabunge na vijana wengi kutoka upinzani ni mwendelezo wake wa kupokea wananchi wa sehemu mbalimbali wanaotaka demokrasia ya kweli.
Meck ambaye alikabidhiwa kadi ya uanachama jana hiyohiyo, alisema ameamua kuhamia ACT kwa sababu vyama alivyopita havikuwa na demokrasia na mabadiliko ya kweli.
Alisema baadhi ya vyama vya siasa havijajikita katika kutoa elimu kwa wanachama wake na kwamba ACT imedhamiria kuirudisha nchi katika misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa.
“ACT kipo tofauti na vyama vingine, leo (jana ) nimejiunga na nimepewa vielelezo ambavyo ni kama mwongozo kwa kile kinachofanywa,”alisema Meck.
Mbali na mwanachama huyo, pia aliyewahi kuwa mlinzi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Khalid Kagenzi naye alionekana katika ofisi hizo.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kama amehamia alijibu: “Ni haki ya kila Mtanzania kujiunga na chama chochote cha siasa anachokitaka. Bado sijachukua kadi yangu ya uanachama,” alisema Kagenzi.
No comments :
Post a Comment