Thursday, July 16, 2015

KUNANI UKAWA?


Wakati hali ya sintofahamu kuhusu hatima ya mgombea Uraisi wa UKAWA ikiendelea Chama cha Wananchi CUF kimekanusha taarifa zilizoenea kuwa kimejitoa kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) .

CUF imesema kuwa haikuhudhuria katika kikao cha Ukawa kilichoendelea juzi kwa sababu kwanza hawakupata taarifa na pia walikuwa na kikao cha ndani ya chama kama katiba yao inavyotaka.

Akizungumza na waandishi jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Magreth Sakaya alisema taarifa za wao kujitoa Ukawa ni za uzushi. Sakaya alisema CUF haikuweza kushiriki kikao cha juzi kutokana na sababu za kikatiba ndani ya chama. “Katika chama chetu tunaendelea na vikao, maamuzi magumu ya chama huamuliwa na vikao vya juu vya maamuzi ndani ya chama,” alisema Sakaya.
Aliongeza kuwa Baraza Kuu la CUF litakutana Julai 25 kutoa maamuzi ili wanaposhiriki vikao vya Ukawa wawe kitu kimoja kama chama. “Maamuzi magumu ya chama huamuliwa na vikao vya maamuzi ndani ya chama, chama chetu kimekuwa kikiendelea na vikao vya ndani ili kuwa na maamuzi ya pamoja,” alisema. Ukawa jana walikuwa na kikao kilichodumu kwa takribani saa 14 na walitoa taarifa kuwa wameafikiana juu ya mgombea wa Ukawa hata hivyo atatangazwa baada ya siku saba.

No comments :

Post a Comment