Tuesday, July 14, 2015

LEO HAPATOSHI; HUKU MAGUFULI KULE DR. SLAA

Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wanatarajia kumtangaza rasmi mgombea wao wa uraisi atakaye peperusha bendera ya umoja huo .

Ukawa inaundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na NLD.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya vikao vya Ukawa vilivyofanyika mfululizo mwishoni mwa wiki, pamoja na mnyukano uliokuwapo, hatimaye vyama hivyo vinatarajia kutoka na jina moja la mgombea urais.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Ukawa, Benson Kigaila, alisema tangu awali Chadema walishakubaliana kwamba mgombea wao ni Dk. Slaa.

“Ndani ya Ukawa kinachofanyika ni maridhiano tu. Kwa Zanzibar tuliridhiana tuwaachie CUF na wao waliridhia kuiachia Chadema Tanzania Bara. Kwa hiyo kinachofanyika kwa sasa ni maridhiano ya ndani ya vyama,” alisema Kigaila.

Kuhusu Dk. Slaa kutochukua fomu kuomba kugombea urais ndani ya chama kama ilivyofanyika kwa viongozi wengine wa Ukawa, Kigaila alisema ni utaratibu wa chama chenyewe.

“Tunapokutana kwenye vikao vya Ukawa si lazima waonekane wote wawe na fomu za kuomba urais, kila chama kina utaratibu wake,” alisema.

Wakati Ukawa wakijiandaa kuliweka hadharani jina la Dk. Slaa leo hii, huenda jiji la Dar es Salaam likawa na chereko katika kila kona kwani siku ya leo Chama Cha Mapinduzi pia kimepanga kumtambulisha mgombea wao, Dk. John Magufuli kwa wananchi wa Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa mwishoni mwa Mkutano Mkuu wa CCM mjini Dodoma jana mchana, baada ya Dk. Magufuli kutambulishwa kwa wakazi wa Dodoma jana jioni, kesho itakuwa ni zamu ya wakazi wa Dar es Salaam.

Magufuli ameteuliwa kuiwakilisha CCM katika kugombea urais baada ya kuwashinda Dk. Asha Rose Migiro na Amina Salum Ali kwenye Mkutano Mkuu.

No comments :

Post a Comment