Wednesday, July 22, 2015

MACHALI AKABIDHIWA KADI YA ACT-MAENDELEO

                       Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto
Kasulu. Mbunge wa Kasulu Mjini ,Moses Machali amekihama rasmi chama hicho na kujiunga na ACT - Wazalendo huku akiwaeleza wananchi waliofika kumsikiliza katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kiganamo mjini hapa kuwa hatasita kuachana na chama chake kipya endapo kitaonekana kinatetea mafisadi na viongozi wanaokandamiza demokrasia.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi na kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe, Naibu Katibu Mkuu huyo wa NCCR - Mageuzi alisema amejiunga baada ya viongozi wa chama hicho kumhujumu katika harakati zake za kutetea masilahi ya Halmashauri ya Wilaya Kasulu.
“Nilijiunga na NCCR-Mageuzi nikitokea Chadema mwaka 2010 na wananchi mkanichagua kuwa mbunge wa Kasulu Mjini ili tushirikiane kupigania haki na maendeleo ya Kasulu, lakini kwa muda mrefu nimekuwa nazushiwa maneno kwamba mimi ni mkorofi na ndiyo maana sielewani na wataalamu pale halmashauri, lakini vita yangu ilichochewa na kuchukia kwangu rushwa na ufisadi, mambo ambayo kuna wenzetu kule NCCR wanashiriki kuyafanya,” alisema.
Alisema: “Nilifukuzwa bungeni pamoja na wabunge wengine watano wa upinzani kwa vile tulikuwa tunapinga kitendo cha Serikali kuleta miswada muhimu kwa hati ya dharura. Kama Spika, Anne Makinda mwenyewe alikuwa anaogopa muziki wangu, hawa watendaji wa Halmashauri wataniweza? Alitamba Machali.
Mbunge huyo alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kueleza namna baadhi ya viongozi wa NCCR walivyokuwa wakitumika kuhujumu miradi ya maendeleo, akimtaja mmoja wa madiwani wa Kasulu kama chanzo cha matatizo ndani ya chama hicho.
Zitto afichua
Akizungumza katika mkutano huo, Zitto licha ya kuwataka wananchi wa Kasulu kujiunga na chama hicho, alisema Machali alishajiunga nao muda mrefu na kwamba alichokuwa anasubiri ni kukabidhiwa kadi. “Tulisema lazima tupate baadhi ya wabunge na viongozi maarufu kutoka vyama vingine, sasa tumeanza na Machali na wengine watafuata,” alisema Zitto.
Viongozi wengine waliojiunga na chama hicho jana ni pamoja na kada wa CCM, Emmanuel Mbwiliza aliyewahi kuwa Diwani wa Kata ya Nyumbigwa hadi mwaka 2010 pia akiwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kuanzia 2007 hadi 2012.
Katika mkutano huo pia viongozi wengine wa NCCR kutoka Kasulu Mjini na Kasulu Vijijini walijiunga na ACT huku wakiahidi kupambana kuhakikisha wanashinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Baadhi ya wananchi hao walionyesha kumuunga mkono Machali katika harakati zake za kutetea Jimbo la Kasulu Mjini kupitia chama chake kipya wakisema watafanya hivyo kutokana na hulka yake ya kupambana na viongozi wanaoonekana kufuja mali ya umma.

No comments :

Post a Comment