Friday, July 24, 2015

SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU BVR


Serikali imetoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika zoezi la uandikishaji wa wananchi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura katika mfumo wa BVR lililoanza juzi jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa Wa Dar es salaam Said Meck Sadiki Amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Manispaa za jiji la Dar es Salaam wanaendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye baadhi ya vituo kufuatia mashine za BVR kushindwa kufanya kazi vizuri.

Amesema kuwa kumekuwa na malalamiko yanayotolewa na wananchi yanayosababishwa na waandikishaji kuchelewa kufika katika vituo walivyopangiwa na kusababisha wananchi kusubiri muda mrefu bila kuandikishwa.

Amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kuhusika na uzembe huo.

Amewaagiza Wakurugenzi wa Manispaa zote za jiji la Dar es Salaam kuwafuta kazi watendaji wazembe ili kuepusha madhara na vurugu zinazoweza kuepukika.

Ameongeza kuwa kuwa kazi ya uandikishaji wananchi inatakiwa kuanza saa 2 asubuhi mpaka saa 12 jioni kila siku kwa tarehe zote zilizopangwa.

Amesema kuwa tayari ameshapokea taarifa za uwepo wa baadhi ya wasimamizi wasio waaminifu wanaokiuka kanuni na taratibu kwa kuwaingiza waandikishaji wasiohusika kusimamia zoezi hilo na kuahidi kulifuatilia suala hilo yeye mwenyewe ufuatiliaji ili sheria ichukue mkondo wake kwa yeyote atakayebainika kuvuruga zoezi hilo.

Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika kuhusu pindi wanapobaini hujuma ya aina yoyote inayolenga kuvuruga zoezi hilo na kuwataka waendelee kujitokeza katika vituo vya uandikishaji ili kutimiza lengo la kuwaandikisha wakazi wote wa Dar es Salaam wenye sifa za kupiga kura.

Pia amevitaka vyama vya siasa kuacha kutumia mwanya huo kuweka bendera au kuvaa mavazi yanayoashiria kampeni za siasa ili kuepusha vurugu.


No comments :

Post a Comment