Monday, July 20, 2015

WAPINZANI WAITOLEA UVIVU SERIKALI KUTOKANA NA MAGUFULI KUTUMIA NDEGE YA SERIKALI

Dar es Salaam. Wanasiasa wa upinzani nchini wamepinga kitendo cha mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kutumia ndege ya Serikali kwenye shughuli za kichama za kujitambulisha wakisema hatua
hiyo ni matumizi mabaya ya rasilimali za Taifa.
Dk Magufuli, juzi alikwenda Mwanza kwa ziara maalumu ya kujitambulisha akitumia ndege ya Serikali aina ya Fokker F28, jambo ambalo limeibua hisia tofauti.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema walifuata taratibu zote kuikodi ndege hiyo na kwamba chama chake ni kikubwa na hakiwezi kushindwa kukodi usafiri huo.
“Ile ni ndege ya Serikali, yeyote anayetaka kuitumia aende kulipia tu, atapewa. Sisi tumekwenda kama wateja wa kawaida tukalipia, ukitaka kujua ni kiasi gani kawaulize wahusika watakueleza,” alisema Nape.
Kuhusu suala hilo la gharama, Kapteni Mhaiki alisema gharama ya kukodi ndege hizo zipo tofauti kutokana na aina inayohitajika akisema aliyoitumia Dk Magufuli inagharimu Dola za Marekani 4,000 sawa na Sh8.4milioni kwa saa moja.
Akizungumzia suala hilo jana, Kiongozi wa chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe alisema viongozi wa Serikali wamekuwa na utamaduni wa kutumia mali za umma kwa shughuli za kisiasa na kusahau kwamba rasilimali hizo ni za Watanzania wote bila kujali itikadi zao.
Zitto na Mbowe
Zitto alisema jambo hilo halijaanzia kwenye ziara ya Dk Magufuli, bali hata mawaziri wote waliochukua fomu walitumia magari ya Serikali kuzunguka nchi nzima kutafuta wadhamini wao kwa nafasi ya urais.
“Jambo hili si kwa CCM pekee, tunaona pia gari la Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB), likitumika kwenye mikutano yake ya kichama. Lile ni gari la Serikali; kwa hiyo lazima tuupige vita utamaduni huu,” alisema Zitto. Alisema CCM ina wajibu wa kuwaeleza Watanzania sababu za kutumia ndege ya Serikali na kama wamelipia fedha ni kiasi gani kilicholipwa huku akisisitiza kuwa utamaduni huu uliokithiri unaligharimu Taifa.
“Mali za umma lazima zitumike kwa shughuli za Serikali na siyo shughuli za kichama. Hili halina upinzani wala CCM, ni jambo linalotakiwa kupigwa vita kwa nguvu zote ili rasilimali zetu zitumike ipasavyo,” alisisitiza kiongozi huyo.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema limekuwa ni jambo la kawaida kwa CCM kutumia vyombo vya Dola katika kufanikisha mambo yao na kwamba sababu za kwamba ndege za Serikali zipo wazi kwa umma ni ‘danganya toto’ ili kufurahisha wananchi.
“Eti ndege hizo zinaweza kukodiwa na mtu binafsi au chama, nani kakwambia? Nenda kakodi kama utapata. Ukweli ni kwamba Magufuli hakuikodi hiyo ndege, kama ni kweli wamekodi watuonyeshe walilipaje?” alihoji Mbowe na kuongeza. “Chadema haijawahi kwenda kukodi kwa sababu ina uhakika haitaipata, hasa ikizingatiwa viwanja tu vya michezo vinavyomilikiwa na CCM havijawahi kutolewa vitumike kwa mikutano ya upinzani tangu mfumo wa vyama vingi uanze zaidi ya miaka 20 iliyopita.”
Mwenyekiti huyo wa Chadema, alisema hata polisi, mahakama na vyombo vya habari vya Serikali vimekuwa vikitumika vibaya kuilinda CCM iendelee kukaa madarakani.
Alipoulizwa juu ya gari la Serikali analotumia kuonekana kwenye mikutano yake ya kisiasa alijibu:  “Nilipopewa gari na Serikali lilikuwa ni kwa matumizi ya upinzani, mikutano ya kisiasa ninayohudhuria ni sehemu ya kazi za upinzani… sasa wanaohoji walitegemea nitalitumia gari hilo kwa ajili ya Serikali? Nenda kawaambie habari ndiyo hiyo na Bunge likivunjwa nitalirudisha.”
Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Constatine Akitanda alisema ana shaka kubwa iwapo ndege hiyo ilikodiwa na CCM na kulipiwa gharama zinazotakiwa.
“Sisi tuna uhakika gani kuwa CCM walikodi? Hata hizo fedha tukisema twende tukaangalie je, ni kweli wamelipa au wamechukua tu hiyo ndege?… hata ukisema tukafanye ‘auditing’ (ukaguzi) hutakuta kitu pale,” alisema Akitanda.
Ufafanuzi wa wakala
Katika ufafanuzi wake, Kapteni Mhaiki alisema hakuna haja ya suala hilo kuchukuliwa kisiasa. “Jukumu la kwanza ni kubeba viongozi wa Serikali lakini kama kuna muda wa ziada tunawahudumia watu wengine kibiashara na huwa tunasafirisha hata timu za mpira na wageni kutoka nje ya nchi wanapotembelea nchini. Mtu yeyote anaruhusiwa kuomba kuikodi, atapatiwa ankara yake… hata awe CUF, Chadema au chama chochote kile kama kuna nafasi anapata,” alisema.

No comments :

Post a Comment