Sunday, August 2, 2015

CHADEMA YATOA TAMKO KUHUSU HABARI ILIYOCHAPISHWA NA RAIA TANZANIA KUMUHUSU DR. SLAA

Ziko habari za uzushi kuhusu Katibu Mkuu Dk. Slaa, zinaandikwa na kuenezwa na Gazeti la
Raia Tanzania kwa siku kadhaa mfululizo sasa.

Uongo huo wa Raia Tanzania leo umeendelea kwa kiwango cha juu zaidi kiasi cha gazeti hilo kuandika kuwa eti Katibu Mkuu Dk. Slaa amekabidhi nyaraka za chama kwa dispatch saa 3 usiku juzi.

Wakuu, hakuna uongo uliokubuhu kama huo. Mtakumbuka uongo huo wa kwamba KM Dk. Slaa anarudisha mali za chama zilienezwa usiku wa juzi mitandaoni na mmoja wa waandishi wa habari aitwae Manyerere Jackton.

Kwa bahati nzuri wakati Jackton (mtu ambaye tunaheshimiana kwa sababu ya kikazi na kitaaluma) wakati akijipatia jukumu la kuandika uzushi badala ya habari na kusambaza uongo badala ya taarifa, binafsi nilikuwepo ofisini physically. Nilikanusha kupitia Jamii Forums ambako alidanganya kwa jina lake, huku 'akijiapiza'.

Uongo huo ambao leo umeshadidiwa na Gazeti la Raia Mwema leo, ulisababisha taharuki isiyokuwa ya lazima kwa waandishi wa habari kadhaa ambao walinitafuta (si Raia Tanzania wala Jackton) na nikawaruhusu waje Ofisini wakitaka usiku huo ili waone namna ambavyo wako watu au chombo cha habari kinaweza kujivika kazi ya kusambaza uongo. Kujeruhi na kuua ukweli.

Kazi ya kujeruhi na kuua ukweli hufanywa sana na maadui wakati wa mapambano kama ilivyo sasa katika mchuano wa kisiasa unaoendelea nchini kuelekea Uchaguzi. Maadui wa CHADEMA wako kazini. Lilitarajiwa hilo.

Wakati Raia Tanzania wakikoleza uongo wao kwa kusema eti 'majira ya saa 3.15 hivi' lilifika Gari aina ya Noah maeneo ya ofisini kisha eti watu wawili wakaingia ofisini wakiwa na mkoba mwekundu, muda huo mimi nilikuwa Ofisini. Hakuna kitu cha namna hiyo kilichofanyika. Labda kama Ni Kwenye Ofisi za gazeti hilo.

Naandika haya nikiwa na uchungu. Kwa sababu huwa sijisikii vizuri kabisa kulumbana na wenzangu (senior fellas) kwenye taaluma ya habari. Tena kwenye mambo ya hovyo yanayohusu kuvunja vunja kabisa misingi ya uandishi wa habari i.e accuracy, facts, truth, objectivity etc.

Inapofikia hatua Gazeti kama hilo linashindwa kabisa kusimama kwenye kitu kiitwacho Social Responsible Journalism inatia aibu na kichefuchefu kwa jamii ya watu makini wanaotaka ushindani wa kisiasa unaoendelea nchini ufanyike kwa misingi ya kila mdau kutimiza wajibu wake inavyotakiwa. Uwajibikaji.

Nimalizie kwa kusema yafuatayo; Katibu Mkuu hajajiuzulu. Nafasi yake haiko wazi kama ambavyo gazeti limepotosha.

Agenda ya kuandika uzushi na uongo kuhusu Katibu Mkuu Dk. Slaa na CHADEMA wanayotekeleza Gazeti la Raia Tanzania walioko nyuma yake wanajulikana. Ni agenda ya CCM na Mawakala wao. Wasaliti wa mabadiliko ambao hawajaamini kuwa ndege ya mabadiliko hatimaye inaruka wakiwa wametupwa nje kwa sababu ya usaliti wao wa kufanya kazi za CCM wakiwa ndani ya CHADEMA kabla hawajatimuliwa.

Mojawapo ya malengo ni kuwachanganya wanachama, wapenzi, mashabiki na wafuasi wa CHADEMA katika kipindi hiki muhimu kinachohitaji utulivu wa mwili, akili na roho ili kupanga mikakati ya kumdhibiti adui na kuweka kila kitu sawa kwa ajili ya kusaka ushindi kwenye Uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Inaitwa diversion. Ili badala ya kuendelea kuwa focused kwenye masuala ya msingi eti tuanze kukimbizana na propaganda!

Aidha, baada ya CCM kusambaratikia Dodoma na sasa iko vipande vipande ikiwa ni mwendelezo wa kuanguka kwa 'himaya' hiyo huku Wananchi wakipandisha mori wa mabadiliko kupitia BVR, lengo jingine ni kutaka kuuhadaa umma wa Watanzania kuwa eti CHADEMA nayo imegawanyika. Wanaota.

Mgawanyiko wa chama cha siasa huwa unatokea kwenye vikao pale ambapo maamuzi yanashindwa kufanyika au kufukiwa. Hakujawahi kutokea jambo la namna hiyo ndani ya chama.

Kwa sababu chama kimejenga utamaduni wa kusimamia misingi katika kusimamia na kuendesha masuala yote, kinaendelea kuwa imara kadri tunavyosonga kuelekea Uchaguzi mkuu.

Uimara huu wa CHADEMA kikijiandaa (kwa kushirikiana na vyama wenza katika UKAWA) kwenda kushinda Uchaguzi, kushika dola na kuongoza serikali, ni mpango wa Mungu. Tujiandae kwa propaganda kubwa zaidi ya hizo za Raia Tanzania.

Tutashinda.

Makene

No comments :

Post a Comment