Wednesday, August 5, 2015

KIKWETE ASAINI MISWADA YA SHERIA YA GESI

Rais Jakaya Kikwete, amesaini miswada mitano ya sheria, iliyopitishwa na Bunge la 10
Julai, mwaka huu. Katika miswada hiyo imo miswada iliyozua tafrani na kusababisha wabunge 45 wa Ukawa kutimuliwa bungeni na wengine kususia mkutano wa 20.

Katika tukio la kihistoria lililofanyika Ikulu, jana na kuhudhuriwa na mawaziri, watumishi wa wizara na wadau wa mafuta na gesi, Rais alisaini miswada hiyo baada ya mawaziri husika kuwasilisha maelezo ya miswada hiyo.

Miswada hiyo ni wa sheria ya mafuta, sheria uwazi na uwajibikaji katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia, muswada wa sheria ya mapato yatokanayo na mafuta na gesi pamoja na muswada wa sheria ya Tume ya walimu.

Vile vile muswada wa sheria ya usimamizi wa masoko ya bidhaa yote ya mwaka 2015.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema tukio hilo ni la kihistoria kwa Tanzania kwa miswada mitano kusainiwa katika hadhara kubwa ya watu.

Alisema miswada ya sheria ya gesi na mafuta inaweka utaratibu mzuri wa kimfumo, kisheria na udhibiti mzuri wa kusimamia uchumi wa gesi na mafuta, kujibu kilio cha Watanzania kuwa rasilimali ziwanufaishe na kizazi kijacho.

Balozi Sefue alisema pia watanzania wataunganishwa na ulimwengu wa gesi kwa biashara watakazoanzisha na kutekeleza katika uchumi huo, ikiwa ni pamoja na kuwa na uchumi nyumbulifu katika kulinda mahitaji ya vizazi vijavyo na cha sasa.“Tunafanya walichofanya wengine duniani na kuepuka yaliyoleta matatizo katika nchi nyingine,” alisema Balozi Sefue.

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema muswada wa sheria ya mafuta unalenga kuleta sheria mpya ya kusimamia sekta ndogo ya mafuta nchini kwenye masuala ya utafutaji; uendelezaji; uzalishaji; usafirishaji; uagizaji; uchakataji; uhifadhi na biashara ya mafuta na gesi asilia nchini.

“Malengo ya muswada wa sheria ni kuimarisha usimamizi wa sekta ili kuhakikisha maslahi ya nchi katika tasnia ya mafuta yanalindwa kikamilifu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo, kuweka mfumo madhubuti wa kisheria utakaoimarisha usimamizi wa shughuli za mafuta katika mkondo wa juu, wa kati na wa chini kupitia sheria moja,” alisema na kuongeza:

“Masuala muhimu ni kuweka utaratibu ambao serikali ya Muungano na ya Mapinduzi ya Zanzibar zitashirikiana katika shughuli za utafutaji, uchimbaji na uendelezaji wa vitalu vya mafuta na gesi katika yaliyo kwenye maeneo yanayugusa pande zote mbili,” alibainisha.

Simbachawene alisema sheria hiyo itawezesha kuanzishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (Pura) ambayo itasimamia shughuli zote za udhibiti katika masuala ya kiufundi na kibiashara katika mkondo wa juu.

Jingine ni kuipa hadhi Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuwa kampuni itakayoshiriki katika shughuli za mafuta katika mkondo wa juu, wa kati na wa chini, kuipa haki ya kipekee TPDC ya kupewa leseni za utafutaji na uzalishaji mafuta na gesi asilia na kukusanya, kununua na kusambaza gesi asilia kwa watumiaji nchini.

Waziri huyo alisema muswada wa sheria ya uwazi na uwajibikaji una madhumuni ya kuweka utaratibu wa upatikanaji kwa wakati taarifa sahihi za malipo, mapato, mauzo na gharama za uwekezaji kutokana na shughuli za madini, mafuta na gesi asilia; kuimarisha uwazi na uwajibikaji wa serikali na kampuni za madini,mafuta na gesi asilia katika kutoa taarifa za malipo, mapato na gharama za uzalishaji. Alisema pia ni kuimarisha mfumo wa utoaji na uwekaji wazi taarifa na taarifa za malipo, mauzo na gharama za uwekezaji katika shughuli za madini, mafuta na gesi asilia, hivyo kuongezeka kwa mapato ya serikali.

Simbachawene alisema mambo muhimu katika muswada ni kuweka vifungu vya adhabu kwa yeyote atakayeshindwa kuwasilisha nyaraka au taarifa zinazotajwa chini ya sheria na atayewasilisha taarifa za uongo.

Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya, akiwasilisha maelezo ya muswada wa sheria ya mapato yatokanayo na gesi na mafuta, alisema katika kuhakikisha Watanzania wananufaika na mapato hayo utaanzishwa mfuko wa fedha hizo ambao utakuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment