Saturday, August 15, 2015

NYAMA YA PUNDA YAZUA KIZAA ZAA DODOMA

Baraza la taifa la usimamizi wa mazingira {NEMC} limekifungia kiwanda cha Huwa Cheng Company Limited
kilichopo mjini Dodoma na kukitoza faini ya shilingi milioni 200 baada ya kubaini kiwanda hicho kinajihusisha na usindikaji wa nyama ya Punda kinyume na utamaduni wa watanzania huku mazingira yake yakiwa hatarishi kutokana na uchafu unaozalishwa kuzagaa kwenye makazi ya watu.


Mabishano makali baina ya wamiliki wa kiwanda hiki raia wa uchina na maofisa wa NEMC yaliyochukua muda mrefu kabla ya maofisa hao kutoa tamko la kufungwa kwa kiwanda hicho ambacho mbali na kuzalisha nyama ya Punda ambayo ni kinyume na utamaduni wa watanzania lakini pia mazingira ya uzalishaji wake ni hatarishi kwa afya za wafanyakazi na majirani wa eneo hilo.

Kiwanda hiki ambacho kwa siku kinadaiwa kuchinja Punda wasiopungua 200 inaelezwa kuwa mbali na kukiuka utamaduni lakini pia kinaharibu kizazi cha wanyama hao ambao uzao wake unatajwa kuwa ni mdogo hali inayotishia wanyama hao ambao kwa kanda ya kati hutumiwa katika kazi mbalimbali kupungua ama kutoweka kabisa.

Mohamed Hamis ambaye ni meneja msaidizi wa kiwanda hiki akizungumza kwa niaba ya raia hao wa uchina anasema nyama hizo za Punda zinasafirishwa kwenda kuuzwa nchini China.

Baadhi ya wananchi wakazi wa Dodoma wameonyesha wasiwasi kwamba huenda nyama hiyo ya punda inapenyeza sokoni na kuuzwa kwenye mabucha na hata kwenye mahoteli na nyama choma kwani ni vigumu kwa mlaji kuitofautisha na nyama zingine wanazotumia.


No comments :

Post a Comment