Dar es salaam: Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amekanusha taarifa za kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa Chama hicho Profesa Ibrahim Haruna Lipumba.
Amesema akiwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, hajapokea taarifa zozote za kujiuzulu kwa Prof. Lipumba, na kwamba hadi saa nne za usiku wa jana Jumatatu ya tarehe 03/08/2015, alikuwa na mazungumzo ya faragha na Prof. Lipumba na wala hajamzungumzia juu ya jambo hilo.
Maalim Seif ametoa taarifa hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, wakati akihutubia kwenye mkutano Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, ambao umewajumuisha pia viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA.
Amesema kwa mujibu wa Katiba ya CUF, kiongozi yeyote wa Kitaifa wa Chama hicho iwapo ataamua kujiuzulu, anatakiwa kuiandikia barua mamlaka iliyomchagua ambayo ni Mkutano Mkuu wa Chama hicho, lakini akiwa katibu wa Mkutano huo, bado hajapokea taarifa hizo.
Amefahamisha kuwa gazeti lililochapisha taarifa hizo katika toleo lake la leo tarehe 4/8/2015 lilikuwa na malengo maalum ya kuvuruga Muungano wa vyama vinavyounda UKAWA, na kwamba malengo hayo hayatofanikiwa.
Katika hatua nyengine Mkutano Mkuu wa Chadema umempitisha kwa kauli moja Waziri Mkuu mstaafu Mhe. Edward Lowassa kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama hicho, na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Mhe. Juma Duni Haji kuwa mgombea mwenza kupitia Chadema.
Mkutano huo pia umeridhia Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad kuwa mgombea pekee wa urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi CUF, kwa kuwakilisha vyama vinavyounda UKAWA ambavyo ni CUF, CHADEMA, NCCR MAGEUZI na NLD.
No comments :
Post a Comment