Sunday, August 2, 2015

Wasomi waelezea tetesi za Dk. Slaa kujiuzulu siasa


Wakati uvumi wa kujiuzulu cheo na kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema),  Dk. Wilbroad Slaa, ukiwa umetawala kupitia mitandao ya kijamii na magazeti, taarifa zinadai kuwa sababu ya kuchukua hatua hiyo ni shinikizo kutoka kwa mkewe.

Taarifa zilizochapishwa na gazeti moja likimnukuu Dk. Slaa mwenyewe, zilisema ameachana na siasa na kujivua wadhifa wake na atabaki kufanya shughuli zingine.

Dk. Slaa  amedaiwa hakubaliani na namna chama chake kilivyompokea Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.

Lowassa aliyekuwa Mbunge wa Monduli alitangaza kuhamia Chadema, Julai 28, mwaka huu  baada ya kutoridhishwa na mchakato wa CCM wa kumpata mgombea wa urais.

Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu vya habari ndani ya Chadema zinadai, Dk. Slaa alishiriki katika mchakato mzima wa kumpokea na kuridhia Lowassa, kusimamishwa kuwa mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Hata hivyo, chanzo kingine cha habari kinadai kuwa mke wa Dk. Slaa, Josephine Mashumbusi, alitoa shinikizo kwa mumewe la kujiuzulu baada ya kuruhusu kusimamishwa mgombea mwingine (Lowassa).

"Josephine alikuwa na uhakika mume wake ndiye atakayesimama ugombea urais kwa upande wa Ukawa, hali ilivyobadilika, akakasirika na kumwambia mumewe ama yeye au Chadema," chanzo kilidokeza.

Kupitia ujumbe uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii, unaoonyesha kutoka kwa Mashumbusi, aliandika "Ni kweli Frida na kwa hili Dk. Slaa amejivua wadhifa wake wa ukatibu mkuu na kuachana na siasa. 

Hamtamsikia tena kwani hawezi kupinga anachokiamini". 
Hata hivyo, Dk. Slaa alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi kuthibitisha madai hayo, iliita mara moja na kuzimwa. Juhudi za kumpata ziligonga mwamba baada ya simu yake kutopatikana hali kadhalika simu ya Mashumbusi.

Wakizungumza na NIPASHE, baadhi ya wasomi walisema kama Dk. Slaa amejiuzulu nafasi yake  na kujivua unachama atakuwa amejijengea heshima na uaminifu na kwamba Chadema kitapata pigo.

Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema  kwa upande wake aliamini kitu kama hicho kitatokea kutokana na tukio hilo kuwa la haraka na kulifananisha sawa na mapinduzi ya ghafla ndani ya chama.

“Nafikiri kama kweli Dk. Slaa amejivua uanachama itakuwa ni jambo zito na pigo kwa Chadema, lakini ni uamuzi wa busara na kumjengea heshima kwa jamii,” alisema Dk. Bana.

Alisema kitendo cha Lowassa kuhamia chama hicho kwa haraka kilileta mashaka na mijadala kwa baadhi ya viongozi.

“Ninavyojua mimi ndani ya Chadema kuna watu wenye misimamo na wapo tayari kuilinda kwa nguvu zote, kujitoa kwake sawa na kutaka kusimamia kile anachokiamini na kukaa kwake kimya katika jambo hili lazima kutakuwa na mshindo mkuu,” alisisitiza.

Mhadhiri huyo alisema anaamini Slaa aliweza kukifufua chama hicho mwaka 2010 kwa kuweka misingi yake ya kukemea ufisadi, hivyo hawezi kurudi nyuma kwa kuivunja. 

Dk. Kitlya Mkumbo kwa upande wake alisema anaheshimu maamuzi ya pande zote mbili kwani zinaonyesha demokrasia na ukomavu wa kisisa.

Alisema Dk. Slaa amechukua uamuzi sahihi wa kujiuzulu kwa sababu ni haki yake kikatiba na Chadema wamechukua hatua ya kumkaribisha Lowassa walikuwa na njia njema kukuza upinzani na kuiondoa CCM madarakani.

KAULI ZA SLAA DHIDI YA LOWASSA
Septemba 15 mwaka 2007 katika viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa alimtaja Lowassa kuwa miongoni mwa mafisadi 11 waliochota fedha Benki kuu katika akaunti ya Epa.

Kauli hiyo alikuwa akiitamka kila mahali alipokwenda na  kusisitiza kwamba Lowassa na viongozi wenzake wa CCM wamechafuka kwa ufisadi.

Akiwa katika kampeni ya urais mwaka 2010, Wilayani Monduli Dk. Slaa alimshambulia Lowassa, kwa kushindwa kudhibiti vitendo vya kifisadi vilivyotokea jimboni na serikalini.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika viwanja vya Bomani, alisema binafsi hana ugomvi  na Lowassa kwani ni mmoja  wa viongozi aliofanya nao kazi kwa karibu na ni rafiki yake, lakini wanatofautiana katika masuala ya msingi yanayohusu maslahi ya Taifa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment