Katibu wa CCM Wilaya ya Mjini Ndg Fatma Shomar, akitangaza matokeo ya uchaguzi wa Kura ya Maoni Jimbo la Malindi Unguja baada ya kukamilisha uchaguzi wake jana. |
Mawaziri wawili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameangushwa katika kura za maoni huku jimbo la Makamo wa Rais pili wa Rais wa Zanzibar likikumbwa na khitilafu katika mchakato wa kura za maoni kupitia Chama Cha Mapinduzi unaoendelea nchi nzima.
Mawaziri walioangushwa katika kura hizo ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Perera Ame Silima.
Mahadhi ameanguka katika mchakato wa kura za maoni jimbo la Paje nafasi ya Ubunge kwa kupata kura 1,785 huku Jaffar Sanya Jussa ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Mkoa wa kusini akiibuka mshindi kwa kupata kura 3,368.
Perera Ame Silima aliyepata kura 1,218 na kubwagwa chini na mpinzani wake ambaye ni Mgombea wa Ubunge Kijana Ussi Pondeza kwa kumpita kwa kura 1,952.
Makamo wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi jimbo lake limekumbwa na mizengwe, hali ambayo ililazimisha kurudiwa kwa uchaguzi huo baada ya kukamatwa masanduku ya kura ambayo yanasadikiwa yalishapigwa kura kabla ya upigaji kura rasmi kuanza.
Hali hiyo ilizusha taharuki na vurugu kubwa huku baadhi ya wapiga kura hao wakitaka masanduku hayo kufunguliwa na kuchomwa moto makaratasi yote na uchaguzi huo uanze tena upya hali ambayo imelazimisha uchaguzi huo kuakhirishwa na kuanza tena upya jana.
Balozi Seif aligombea Jimbo hilo jipya baada ya Jimbo lake la zamani la Kitope kufufutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) katika ugawaji wa mipaka ya majimbo iliyofanyika hivi karibuni.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alikiri kutokea kwa khitilafu katika jimbo analilogombea Balozi Seif la Mahonda na akasema uchaguzi huo umelazimika kurejea kutoka na khitilafu hizo za kiufundi
Vuai alisema maeneo mengine uchaguzi umekwenda vizuri licha ya changamoto za hapa na pale lakini umefanyika kwa uwazi na demokrasi ya hali ya juu kwa wanachama hao kuchagua viongozi wanaowataka bila ya matatizo yoyote.
Aliyekuwa Waziri wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Muungano) na katibu wa Kamati Kuu Idara ya Organizesheni, Mohammed Seif Khatib 1,333 amechuana vikali kwa kupishana kura 1,333 na katika jimbo la Uzini ambapo na mpinzani wake Salum Mwinyi Rehani ameibuka kidedea kwa kupata kura 1,521.
Kwenye nafasi ya Uwakilishi wa Jimbo hilo, Mfanyabiashara Maarufu, Mohamed Raza Daramsi amefanikiwa kutetea nafasi yake kwa kupata kura 4,205 na kumshinda mpinzani wake vibaya sana Yussuf Suleiman aliyepata kura 673.
Mfanyabiashara mwengine ambaye ni ndugu ya Mohammed Raza, aitwaye Ibrahim Raza aliyewania katika jimbo la Kiembe Samaki amembwaga Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM na Katibu wa Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar, Bi Waride Bakari Jabu.
Katika Jimbo la jipya la Paje Mwakilishi wa zamani Jaku Hashim Ayoub amefanikiwa kutetea nafasi yake kwa kupata kura 2,530 dhidi ya mpinzani wake, Radhia Simai Msheli aliyepata kura 931.
Mbunge wa Jimbo la Chwaka aliyeshikilia jimbo hilo miaka 20 kwa vipindi vine Yahya Kassim Issa ameabwagwa chini baada ya kupata kura 1,572 dhidi ya mpinzani wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Baguwanji Mensuriya Baguwanji aliyepata kura 1,951.
Jimbo la Tunguu nafasi ya uwakilishi Simai Mohamed Simai ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamishna wa Tume ya Marekebisho ya Katiba na alitewahi kugombea Jimbo la Mji Mkongwe ameibuka kidedea kwa kupata kura 1,219 na kumshinda aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo, Mussa Ali Hassan aliyepata kura 1,155.
Afisa Mwandamizi wa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, Mtumwa Peya ameibuka mshindi katika kura hizo za maoni za Jimbo la Bumbwini kwa nafasi ya Uwakilishi kwa kupata kura 632 na kumuwacha nyuma sana mpinzani wake Hassan Khamis aliyepata kura 235.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Miundo Mbinu Zanzibar, Issa Haji Ussi aliyewania Jimbo la Chwaka amepata kura 3,959 na kufanikiwa kutetea nafasi bila ya kuwa na mpinzani.
Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sada Salum Mkuya ambaye ni mara yake ya kwanza kuwania nafasi hiyo kupitia katika Jimbo jipya la Welezo ameshinda nafasi ya ubunge
Wakati Sada ameshinda nafasi hiyo Mwanamke mwenzake aliyewania Ubunge wa zamani katika Jimbo la Koani na sasa kugeuzwa Jimbo la Tunguu ameshindwa kutetea nafasi yake hiyo Amina Clement Andrew ambapo amedondoshwa chini kwa kupata kura 905 dhidi ya Mgombea mpya Khalifa Salum Suleiman aliyepata kura 2,394.
Mwanamke mwengine aliyeshindwa kutetea nafasi yake ni Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Thuwaiba Edington Kisasi aliyewania Jimbo la Fuoni ambapo nafasi yake imechukuliwa na mwanamke mwenzake Amina Khamis.
Watoto wawili wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, ambaye ni Waziri wa Ulinzi Hussein Ali Hassan Mwinyi ameendelea kutetea nafasi yake ya Ubunge Jimbo la Kwahani wakati ndugu yake Abass Ali Hassan Mwinyi amewania nafasi ya Ubunge katika jimbo la Fuoni na kuibuka kidedea.
Katika Jimbo la Makunduchi, Waziri wa Kazi Zanzibar anayetetea nafasi ya uwakilishi kwa muda wa vipindi vinne sasa ameibuka tena mshindi kwa kupata kura 4,548 wakati Haji Ameir Haji aliyechukuwa nafasi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Samia Suluhu Hassan ameibuka na ushindi kwa kupata kura 1,754.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana UVCCM Masauni Hamad Masauni amefanikiwa kuitetea nafasi yake katika Jimbo la Kikwajuni kwa kupata kura 2,222 dhidi ya mpinzani wake Mussa Shaali Choum aliyepata kura 461. Masauni atachukua na Salim Mwalimu (Chadema) katika uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Octoba 25 mwaka huu.
Katika Jimbo la Jangombe Ubunge Mgombea Ali Hassan Omar ameibuka kidedea kwa kupata kura 879 dhidi ya mpinzani wake Abdullah Hussein Kombo aliyeambulia kura 639.
Wakati nafasi ya uwakilishi ikishikiliwa na Abdullah Maulid Diwani ambaye amepata kura 740 dhidi ya mpinzani wake Ramadhan Hamza Chande aliyepata kura 441 katika kura hizo za maoni.
Aliyekuwa Waziri Kiongozi Zanzibar na Waziri wa Serikali ya Muungano, Shamsi Vuai Nahodha amebadilisha upepo kutoka kwenye uwakilishi na kuwania Ubunge katika Jimbo jipya ya Kijito Upele na kuibuka mshindi.
Katika kichanganyiro hicho cha kura za maoni Jimbo la Malindi nafasi ya Ubunge imechukuliwa na Abdullah Juma Abdulla kwa kupata kura 558 dhidi ya mpinzani wake Kombo Mshenga Zubeir aliyepata kura 241.
Aidha Jimbo hilo nafasi ya Uwakilishi amekamatwa na Mohammed Ahmada Salum kwa kupata kura 336 na kumbwaga mpinzani wake, Abdulrahman Hassan aliyepata kura 271
Matokeo ni haya;
Mshindi wa Jimbo hilo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Rahaleo ameshinda jimbo la Malindi kama ifuatavyo:-
Mshindi wa kinyangayiro hicho cha Uwakilishi katika Jimbo la Malindi ni:
- Mshindi wa kwanza ni Dr Abdalla Juma Sadala kura 558,
- Mshindi wa Pili Kombo Mshenga Zuberi kura 241
- Mshindi wa Tatu Ndg Mohammed Suleiman Omar kura 168.
- Nafasi ya Nne Ndg Abdi Ibrahim Sanya kwa kupata kura 108.
- Nafasi ya Tano Ndg Ame Ameir Ame amepata kura 25
- Nafasi ya Sita Ndg Said Kheir Ameir amepata kura 17.
- Wa mwisho katika ni Ndg Nassor Khamis Mohammed kura 11.
Mshindi wa kinyangayiro hicho cha Uwakilishi katika Jimbo la Malindi ni:
- Ndg Mohammed Ahmada Salum kwa kura 336.
- Mshindi wa Pili Ndg Abdurahaman M Hassan kura 271
- Mshindi wa Tatu Ndg Himid Mbwana Said kura 254
- Nafasi ya Nne NdgAli Abdalla Suwed (MAKASI)
- Nafasi ya Tano Ndg Ussi Said Suleiman kura 112.
Mshindi wa Jimbo hilo ni sura mpya tayari ameshawahi kugombea Jimbo hilo kwa mara ya pili na kipindi hiki kuibuka mshindi katika nafasi ya Ubunge kwa kumuangusha aliyekuwa mbunge wa Jimbo hilo Ndg Hussein Mussa Mzee.
- Mshindi wa kwanza ni Ndg Ali Hassan Omar King, kura 879.
- Mshindi wa Pili Ndg Abdalla Husein Kombo kura 639.
- Nafasi ya tatu ni Ndg, Hussein Mussa Mzee, kura 566.
- Nafasi ya Nne ni Ndg Talib Ali Talib aliyepata kura 341
- Nafasi ya Tano Ndg Mgeni Mwalimu Ali aliyepata kura 173.
- Nafasi ya mwisho ni Ndg Haji Lila Haji, aliyepata kura 58.
- Mshindi wa Kwanza wa Nafasi ya Uwakilishi Jimbo la Jangombe ni Ndg Abdallah Maulid Diwani kura 740.
- Mshindi wa Pili ni Ndg Ramadhani Hamza Chande kura 441.
- Mshindi wa tatu ni Ndg Othman Shaban Kibwana kura 418.
- Mshindi wa nne ni Ndg Othman Sulieman Nyanga kura 302.
- Mshindi wa tano Ndg Mwatum Mussa Suleiman kura 201.
- Mshindi wa sita ni Ndg Mwarab Mmadi Mwarab kura 169.
- Mshindi wa saba ni Ndg Mohammed Rajab Soud kura 154.
- Wa Nane Ndg Idrisa hussein Mrisho kwa kupata kura 75.
- Nafasi ya Tisa ni Ndg Said Ali Hamad, kwa kupata kura 63.
- Nafasi ya Kumi ni Ndg Shehe Othman Mohammed kura 08
No comments :
Post a Comment