Saturday, August 8, 2015

ZITTO: "WASALITI WA UPINZANI SIYO ACT-MAENDELEO"

KIONGOZI Mkuu wa ACT Wazalendo, Kabwe Zitto amewataka Watanzania wasikubali kugeuzwageuzwa kama chapati na baadhi ya wanasiasa wasioitakia mema Tanzania.

Zitto alisema hayo  juzi mkoani Singida, wakati akihutubia wananchi akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku moja.

Alisema kuwa siku si nyingi, baadhi ya viongozi na wanasiasa wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kumnyooshea kidole aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuwa ni fisadi mkubwa hapa nchini.

“Lakini cha kushangaza, viongozi hao hao wamegeuka na kuanza kumsifia Lowassa kuwa si fisadi, bali ufisadi aliokuwa uko kwenye mfumo wa utawala na wala sio wa mtu binafsi,” alisema Zitto.

Alisema kuwa viongozi hao wamefikia hatua ya kumsafisha Lowassa na ‘kumuuzia’ chama chao bila mkataba na kumpa fursa ya kugombea nafasi nyeti ya urais.

“Haingii akilini kwamba mtu ambaye kwa muda mrefu alikuwa akihusishwa na ufisadi, akasafishika kwa muda mfupi na kuanza kutangazwa kuwa hakuwa fisadi bali ni mfumo wa CCM tu ndio unaohusika na ufisadi huo,” Zitto alishangaa na kuongeza; “Viongozi hao hao walikuwa wakituhumu ACT - Wazalendo kuwa wamesaliti upinzani kwa kufadhiliwa na Lowassa katika uendeshaji wa ustawi wa chama hicho kipya na kwamba kilikuwa kinamwandalia makazi mapya mara atakapoihama CCM,” alisema.

Alisema kuwa anamshukuru Mungu kuwa sasa mambo ni bayana.

“Waliokuwa wakimwandalia makazi mapya ni Chadema na sio ACT –Wazalendo.” Kutokana na hali hiyo, Zitto aliwataka Watanzania kuwa makini na viongozi wanaotaka kuwageuzageuza kama chapati kwani iwapo watakubali kuwa chapati nchi itatumbukia mahali pabaya."

No comments :

Post a Comment