Monday, July 20, 2015

MBUNGE APELEKEWA FOMU NYUMBANI



                                                            Wazee wakimpoelekea fomu ya ubunge Deo Filikunjombe nyumbani kwake kwa maandamano 


WAZEE Ludewa wamemchukulia fomu ya kugombea Ubunge, mbunge aliyemaliza muda wake hivi karibuni, Deo Filikunjombe wakimwomba kuendelea kuongoza jimbo hilo kwa miaka 20 zaidi huku wakidai kuwa kama usingekuwa ni utaratibu wa chama cha mapinduzi (CCM) na ule wa tume ya uchaguzi (NEC) wa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano, basi wao wangempitisha mbunge huyo bila kupingwa na uchaguzi kwa wilaya ya Ludewa ungekuwa wa madiwani pekee na sio kwa urais Dk John Magufuli wala mbunge wao huyo.

Filikunjombe amewaunga mkono kwa kusema anajivunia uchapakazi wa Rais Dk Jakaya Kikwete kwani ni Rais pekee aliyesaidia kuiwezesha Ludewa kusonga mbele na zawadi ambayo wananchi wa Ludewa  wanaitoa kwa CCM ni kuhakikisha mgombea urais wa CCM, Dk Magufuli anapata kura nyingi zaidi ukilinganisha na wilaya yoyote hapa nchini kwani pia amehusika kuwakomboa wananchi wa Ludewa kwa kutengeneza barabara za wilaya hiyo.

Wakizungumza wakati wa kumkabidhi fomu nyumbani kwake Ibani mjini Ludewa wazee hao walisema wamelazimika kumchukulia fomu hiyo na kwenda kumkabidhi baada ya kuridhishwa na kazi kubwa aliyoifanya kwa kipindi cha miaka mitano ambayo amepata kuwa mbunge wa jimbo hilo na kuonyesha utendaji mkubwa zaidi ukilinganisha namaendeleo yaliyoonyeshwa na wabunge 7 waliotangulia katika jimbo hilo .

Hivyo walisema bado wanaimani kubwa na mbunge wao na kuwa imani na matumaini ya wananchi wa Ludewa ni kuona Filikunjombe anaendelea kuwatumikia wananchi hao kwa vipindi vingine 4 kwa maana ya miaka 20 ama kuendelea kuongoza jimbo hilo hadi pale atakapoamua kustaafu mwenyewe kwani utendaji kazi wake wa kazi ndio ambao umemfanya kupewa dhamana hiyo ya kuendelea kuongoza jimbo hilo.

"Tumekuamini na tumependezwa na utendaji kazi wako hivyo wewe tunakubariki kuendelea kuongoza tena na tena jimbo hilo kwani ulipokea likiwa katika hali mbaya na sasa wananchi wa Ludewa kupitia jopo la wazee tumekuamini zaidi na tumekuchukulia fomu hii ya ubunge kama ishara ya kukuamini zaidi ......tulikuita jembe na sasa wewe ni katapila letu Ludewa umeweza kupita pasipo pitika umetufanikishia maendeleo makubwa kwa kipindi kifupi zaidi "

Kwa upande wake mbunge Filikunjombe pamoja na kuwashukuru wazee hao na vijana wa boda boda  zaidi ya 300 katika wilaya ya Ludewa walioungana kumchukulia fomu hiyo alisema kuwa imani kubwa na ushirikiano mkubwa ambao wananchi wa Ludewa wameuonyesha wakati wa utumishi wake umemfariji na kuweza kufanya kazi kubwa zaidi ikiwa ni pamoja na kuwatumikia vema buneni pasipo kusinzia kama walivyofanywa baadhi ya wabunge wengine.

Filikunjombe alisema ili kuwa ni vigumu kwake kusinzia bungeni kutokana na aina ya makubaliano yake na wananchi waliomtuma kwenda kuwawakilisha na kuwa wananchi hao walimtuma kuwasemea bungeni hivyo kama nae angeungana na baadhi ya wabunge ambao uwakilishi wao bungeni ulikuwa ni kusinzia basi wilaya ya Ludewa isingekuwa na maendeleo kiasi hicho.

Alisema kuwa leo hata wale wananchi wa Ludewa ambao walikuwa wakikwepa kuitwa wana Ludewa kutokana na uduni wa maendeleo uliokuwepo katika wilaya hiyo hivi sasa wameanza kutembea kifua mbele kujivunia wilaya yao tofauti na zamani ambapo wengi wao walikuwa wakidanganya kuwa wanatoka mkoa wa Ruvuma.

"Kazi mlionituma bungeni Dodoma nimeifanya zaidi ya uwezo wangu na ndio maana leo wilaya yetu  imepiga hatua kubwa katika maendeleo na ukweli nimefanya yale mlionituma bungeni ombi langu kubwa kwenu wenzangu naomba mzidi kuniombea afya njema zaidi na kuniunga mkoni ili nikirudi bungeni tena kuweza kufanya mengine makubwa zaidi ya haya"

Alisema kuwa hawezi kusema wabunge waliotangulia hawakufanya chochote kabisa katika jimbo la Ludewa japo kila mmoja aliweza kufanya kulingana na uwezo wake ikiwa ni pamoja na mbunge wa kwanza kuleta meli ,mbunge mwingine alileta basi ,mwingine umeme Ludewa mjini lakini kwa upande wake amefanya zaidi ya hayo na kuifanya wilaya hiyo kuwa wilaya ya mfano katika wilaya za mkoa wa Njombe huku akisisitiza kuwa lengo yake ni kuona wilaya ya Ludewa inaendelea kuongoza kwa maendeleo ukilinganisha na wilaya zote za mkoa wa Njombe.

Kwani alisena nia, uwezo na nguvu ya kuifanya wilaya ya Ludewa kuongoza katika maendeleo bado anayo na kuwa kazi kubwa ya wananchi wa Ludewa kuendelea kutoa ushirikiano kwake tena .

Hata hivyo alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika wilaya hiyo kamwe hataacha kumpongeza Rais Dk Kikwete ambae amekuwa sehemu ya mafanikio yake na mafanikio ya wananchi wa Ludewa katika maendeleo ila pia aliyekuwa waziri wa ujenzi Dr Magufuli ambae saa ndie Rais mtarajiwa wa awamu ya tano kwani kati ya mawaziri waliopambana kwa ajili ya Ludewa Dr Magufuli ni namba moja na kuwa zawadi yake ni kupata kura za kishindo katika wilaya hiyo ya Ludewa.

Alisema Rais Dk Kikwete kwa upande wake tayari amekwisha ahadi kufika kuwaaga wananchi wa Ludewa kabla ya kumaliza muda wake kwa kuzindua ujenzi wa viwanda vya chuma katika wilaya hiyo ila pia Dr Magufuli anataraji kufika katika wilaya hiyo ya Ludewa wakati wowote kuanzia sasa hivyo pamoja na kuwashukuru viongozi hao wakubwa kwa upendo wao kwa wana Ludewa bado alisema historia kubwa wameiandika katika wilaya hiyo.

Katika zoezi hilo la wazee kumkabidhi fomu ya ubunge Bw Filikunjombe zaidi ya Tsh 400,000 zikichangwa na wananchi mbali mbali yakiwemo makanisa na watu binafsi pamoja na mbuzi na zawadi nyingine kama sehemu ya kumuunga mkono mbunge huyo katika safari yake ya kugombea tena ubunge wa jimbo hilo la Ludewa.


Msafara wa vijana wa boda boda zaidi ya 300 waliowasindikiza wazee wa Ludewa kumchukulia fomu mbunge Deo Filikunjombe 


Safari ya kuelekea nyumbani kwa Filikunjombe kukabidhi fomu ya ubunge 


Wazee hao wakiwa nyumbani kwa mbunge Filikunjombe kumkabidhi fomu ya ubunge Ludewa 

No comments :

Post a Comment