CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA), kimesema kitaitisha mgomo nchi nzima kama Serikali haitashusha gharama za ushuru zilizopandishwa ghafla.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TABOA,
Ennea Mrutu, alisema Serikali imewataka walipe asilimia 25 ambayo ni kubwa mno.
Alisema awali walikuwa wakilipa asilimia 10 lakini hivi sasa imepanda na kufikia 25 ambazo zitawafanya washindwe kumudu gharama za uendeshaji.
"Basi moja tulikuwa tunalipa ushuru sh. milioni 40, lakini sasa tunatakiwa kulipa sh. milioni 94 ambazo ni kubwaÉtutashindwa kuwahudumia Watanzania," alisema Mrutu na kuongeza kuwa, kama Serikali itaendelea na msimamo huo, kuanzia sasa mgomo wa kusitisha huduma unanukia, tumeleta mabasi mengi yako bandarini, tumeshindwa kuyakomboa.
Aliongeza kuwa, Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2015/16, haikuweka kipengele chochote cha kupandisha gharama za ushuru lakini wanashangazwa na hatua hiyo.
Mrutu alisema, chama hicho kimewaandikia barua Waziri wa Uchukuzi, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Waziri Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Akijibu malalamiko hayo, Waziri wa Fedha, Bi. Saada Mkuya alikiri kupokea barua ya TABOA na kusema Serikali wanaifanyia kazi.
"Nimepokea barua yao, nashangaa kuona wamekuja kwa waandishi wa habari hata kabla hatujazungumza, jambo kubwa ni kwamba, tunashughulikia suala lao...kwa kuwa wametoa tamko kwenu na sisi tunajipanga kutoa taarifa rasmi. Nawaomba wajue tulitoa punguzo kwa mradi wa mabasi ya mwendo kasi tu (DART)," alisema Bi. Mkuya.
No comments :
Post a Comment