Tuesday, August 4, 2015

MANJI APONEA TUNDU LA SINDANO

Mgombea udiwani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM, kata ya Mbagala Kuu, jijini
Dar es Salaam, Yusuf Manji (pichani), anadaiwa kunusurika kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakiwa kwenye harakati za kugawa rushwa na wapambe wake.
 
Inadaiwa kuwa Manji akiwa na wapambe wake, walikuwa wakifuatiliwa na taasisi hiyo baada ya kupata taarifa kuwa mgombea huyo alikuwa katika harakati za kugawa fedha ili achaguliwe.
 
Tukio hilo lilitokea Jumamosi mchana kwenye ukumbi wa Vigae Pub, ambapo mgombea huyo alionekana kukusanyika na wapambe wake na ndipo walipofuatiliwa na taasisi hiyo kujua kinachoendelea.
 
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Temeke, Beutoz Mbwiga, alithibitisha kuwa taasisi yake iliweka mtego wa kumkamata mgombea huyo akiwa na wapambe wake lakini mtego huo haukuzaa matunda.
 
Alisema Manji alikuwa na watu wake pamoja na mabaunsa katika ukumbi huo uliopo Mbagala na gari la Takukuru lilipowasili maeneo hayo, mgombea huyo na wapambe wake walitawanyika katika ukumbi huo.
 
“Watu wetu walipoingia kwenye ukumbi huo kufuatilia walishtuka na walianza kusambaratika, hivyo hawakufanikiwa kumkamata Manji wala wapambe wake….nahisi huenda gari letu lilionekana ndipo wakaanza kutangaziana na kuamua kuondoka ukumbini hapo au huenda wamepewa taarifa kuwa tunakwenda huko,” alisema.
 
Juzi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Mababida, alisema wagombea wa CCM mkoa huo watakaothibitika kugawa rushwa, watanyang’anywa ushindi wao haraka na kupewa wengine wanaowafuatia katika ushindi.
 
Madabida aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotaka kujua uwapo wa malalamiko ya rushwa kwa baadhi ya wagombea wa chama hicho.
 
Alisema wagombea wote na wanachama wamepewa mwongozo kuwa anayetaka uongozi kwa kuhonga hafai kwa kuwa anayefaa hawezi kuhonga na kwamba wanachama wanajua uwezo wake na watamchagua wanayeona anafaa.
 
“Kama wapo waliojaribu kutoa hongo, nimeambiwa wapo walionusurika kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, yeyote atakayethibitika atakuwa amepoteza sifa,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment